KUNI AU UMEME? UTACHOMWA VIPI?

Kuna habari zilizosambaa kote kama moto ulioshika wenyewe na kuviviwa na upepo mkali wa kiangazi katikati ya msitu uliojaa majani makavu. Kumezuka mtindo mpya unaowashtua wengi. Kinyume na mila na desturi tulizo na uzoefu nazo huku kwetu, baadhi ya watu siku hizi wanateketeza maiti zao. Sasa mjadala umeibuka na kushika moto mitaani baada ya kufariki kwa watu kadhaa mashuhuri na miili yao kuchomwa. Inafahamika na wote kuwa tangu kitambo wanaojihusisha na shughuli ya kuteketeza marehemu wao ni wale wanaoshikilia itikadi ya Kihindu na baadhi ya wazungu, kwetu ni jambo la karaha. Jambo geni na limewaacha wengi vinywa wazi.

 

Juzi nilikuwa na malumbano makali yanayoangazia mada hii hii. Ofisini niko na sahibu wangu mmoja anayeunga mkono itikadi hii geni. Aliniaeleza kuwa yeye hana tatizo na uteketezaji wa maiti na kusisitiza kuwa eti hata sisi waafrika zamani tulikwa hatuzikani. Tabia ya kuzika ililetwa na wazungu na waislamu. Mtu akifa alikuwa anachukuliwa na kutupwa msituni aliwe na wanyama wa porini. Loh! Ni kudhalilisha maiti kulioje! Tabia ya kuzika haikuwepo zamani za kale, alishikilia.  Mimi nikamwambia basi hata hiyo ya kuchoma si yetu asli yake ni ya mabaniani na baadhi ya wazungu. Hapo ndio ikawa ni kama nimeongeza mafuta ndani ya moto, akaruka na kuniambia hakuna makosa ya kuchoma eti pia inasaidia kuhifadhi mazingira. Loh vipi? Nikiwa bado nimepigwa na butwaa alizidi kunirushia manufaa ya kuchoma maiti…eti ni haraka na haina gharama kubwa na jivu la aliyeunguzwa uhifadhiwa ndani ya chombo na huwa eti ni rahisi kubebwa na kugawiwa jamaa wa karibu wa marehemu.

 

 

Ninavyojuwa mimi itikadi hii ni kinyume na maadili ya dini za familia nyingi hapa nchini na duniani kote. Kuchoma kunafanya iwe vigumu kwa waliofiwa kuomboleza. Kuzika kunafanya iwe rahisi kwa familia kuzuru kaburi, kumkumbuka na kumuombea mwendazake. Waislamu wanaamini kuwa maiti anastahili kushughulikiwa kwa uangalifu kwa vile anahisi uchungu pia, ata kuoshwa hivyo basi kumchoma maiti ni swala ambalo haliko kamwe. Ni adhabu kubwa sana kwa aliyekufa.