CHAKULA SI CHAKULA TENA!

unnamed (1)

CHAKULA SI CHAKULA TENA!

Nani anayekumbuka maankuli yalivyokuwa zamani? Nikitafakari udogoni wetu tulikuwa tunakula vyakula halisi vyenye ladha na afya…ugali uliosongwa kwa unga wa mahindi yaliyosagwa nyumbani kwa kinu cha kuzungushwa kwa mkono, ukionja sukuma wiki ulihisi unakula mboga za majani mabichi yaliyojaa afya tele, mchuzi ulipokaangwa na kuwekwa nyanya uliipata harufu halisi ya nyanya ukiwa nje ya nyumba, nyama ya ng’ombe yenye ladha ya kutamanisha unapoitafuna kisha tuliteremsha mlo kama huo kwa maziwa ya mtindi matamu ya kukupa sifa kamili. Asubuhi wakati wa kupata kiamsha kinywa, Mama alipotukaangia mayai ladha yake ilikuwa nzuri hata sijawahi kuipata tena ladha kama hiyo.

Samaki hazivuliwi tu katika Ziwa la Victoria pekee, bali kuna zile zinazotoka Uchina…hatuna uhakika ni samaki au ni vitu vilivyotayarishwa kiwandani na kuundwa kama samaki! Maana Wachina wana ubunifu wa hali ya juu. Kuku siku hizi hudungwa sindano za kemikali ya kuzifurisha ili wanunuzi waone kuwa ni kubwa. Hali ya nyama sasa ndio ya kutamausha kabisa, ili zionekane kuwa sawa kwa muda mrefu bila kuoza huwa zapakwa kemikali hatari ya sulphite ambayo yasemekana pia inayotumiwa kuhifadhi maiti. Kemikali hizi zina madhara chungu nzima kwa watu!

Mayai pia hali yake haieleweki kamwe. Mboga zanyunyizwa kemikali za sumu ili kuua wadudu na kuzifanya zipevuke upesi ndio zipate kuwasilishwa sokoni haraka ili wauzaji watengeze faida yao bila ya  kujali madhara kwa wanaadamu wenzao. Habari za Sukari sote twakumbuka ilipogunduliwa kuwa na mercury kisha mabwenyenye wahusika walikamatwa na hatimaye kama kawaida, habari hizo zikafifia na hatujazisikia tena. Kweli nchi yetu ina magwiji wa ufisadi. Maji ya kunywa yanayohifadhiwa chupani almaarufu ‘Mineral Water’ pia yamezusha purukushani baadhi yakisemekana kuwa ni maji tu ya kawaida ya bomba yaliyobandikwa chapa za kuvutia na kuuzwa kama maji safi ya kistaarabu!

Ulafi na kupapia utajiri kutoka kwa baadhi yetu unatufanya tuchanganyikiwe tusitambue nini cha kuliwa.